Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wefaq nchini Bahrain, imelaani uamuzi wa Wizara ya Sheria uliotolewa mwanzoni mwa mwezi Septemba 2026, unaohusiana na kupanga upya vibali vya kutoa mawaidha, kuongoza dini, hotuba na kusoma au kuimba kasida za maombolezo ya kidini. Jumuiya hiyo imesema kuwa hatua hii ni sura mpya katika mfululizo wa vita vya kuangamiza vinavyolenga Mashia.
Jumuiya hiyo imesisitiza katika taarifa yake kwamba uamuzi huo si hatua ya kawaida ya kiutawala, bali ni kiungo kipya katika mfululizo wa hatua zilizopangwa za kuwalenga Mashia, pamoja na mwendelezo wa vita vya kuangamiza vinavyolenga sifa na utambulisho wao wa kidini. Hatua hii imekuja katika mazingira ya vita vikali vinavyoendeshwa dhidi ya Mashia, ambavyo vinajumuisha kuwakamata maulama wao, kuhalalisha kuwachukulia kuwa ni wahalifu kwa kutekeleza ibada zao za kidini, na kuingilia nyanja zote za utambulisho na alama zao za kidini.
Uamuzi wa Wizara ya Sheria umechukuliwa ili kukamilisha lengo la mamlaka la kuuteka na kuumiliki mimbari ya kidini, kupitia kuamua ni nani mwenye haki ya kuzungumza kuhusu masuala ya dini. Hii ina maana ya kuzuia kila sauti ambayo haiimbi sifa za mfumo unaotawala, ili isiweze kutekeleza haki yake ya kiasili ya kufanya ulinganiaji wa dini na kufufua ibada na alama za kidini.
Sharti la kuwa na “tabia njema na mwenendo mwema” (cheti cha mwenendo mzuri) ili kufanya shughuli za utoaji wa hotuba na kusoma au kuimba kasida za maombolezo, ni sharti lisilo na uwazi na lenye utata. Si chochote zaidi ya chombo kamili cha kiusalama kinacholenga kuwaondoa mamia ya wahutubu, waimbaji wa maombolezo na maulama wa dini ambao, kutokana na misimamo yao, wamekuwa wakikabiliwa na kukamatwa kiholela au mashauri ya kisheria yaliyojaa chuki.
Mfumo wa sasa unajaribu kumgeuza mhutubu na mwimbaji wa maombolezo kuwa mfanyakazi wa kawaida tu anayesubiri kibali cha kiusalama kutoka Wizara ya Sheria, au anayesubiri hotuba na mihadhara yake iliyoandaliwa mapema kutumwa kwake kupitia korido za Wizara ya Mambo ya Ndani. Hatua hii inafuta maudhui huru ya ibada na alama za kidini, na kuzigeuza kuwa taratibu za kidini zinazowekwa chini ya uangalizi mkali wa kisiasa.
Maoni yako